1 Kings 20

Ben-Hadadi Aishambulia Samaria

1 aWakati huu, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akakusanya jeshi lake lote. Akifuatana na wafalme thelathini na wawili wakiwa na farasi na magari ya vita, akakwea kuuzingira kwa jeshi Samaria na kuishambulia. 2Akawatuma wajumbe katika mji kwa Ahabu mfalme wa Israeli, kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: 3‘Fedha yako na dhahabu ni yangu, nao wake zako walio wazuri sana na watoto ni wangu.’ ”

4Mfalme wa Israeli akajibu, “Iwe kama usemavyo, bwana wangu mfalme. Mimi na vyote nilivyo navyo ni mali yako.”

5Wale wajumbe wakaja tena na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo Ben-Hadadi: ‘Nimetuma kutaka fedha yako na dhahabu, wake zako na watoto wako. 6Lakini kesho wakati kama huu, nitawatuma maafisa wangu kukagua jumba lako la kifalme na nyumba za maafisa wako. Watatwaa kitu unachokithamini nao watakichukua.’ ”

7 bMfalme wa Israeli akawaita wazee wote wa nchi na akawaambia, “Tazama jinsi mtu huyu anavyochokoza! Wakati alipotuma apelekewe wake zangu na watoto wangu, fedha zangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.”

8Wazee na watu wote wakajibu, “Usimsikilize, wala usiyakubali matakwa yake.”

9Kwa hiyo akawajibu wajumbe wa Ben-Hadadi, “Mwambieni bwana wangu mfalme, ‘Mtumishi wako atafanya yote uliyoyadai mwanzoni, lakini dai hili la sasa siwezi kulitekeleza.’ ” Wakaondoka na kupeleka jibu kwa Ben-Hadadi.

10Kisha Ben-Hadadi akatuma ujumbe mwingine kwa Ahabu, kusema “Miungu iniletee maafa, tena makubwa zaidi, ikiwa vumbi la Samaria litatosheleza konzi moja ya kila mtu ya wale wafuatanao nami.”

11 cMfalme wa Israeli akajibu, “Mwambieni, ‘Yule anayevaa mavazi ya vita asije akajisifu kama yule anayevua.’ ”

12Ben-Hadadi alisikia ujumbe huu wakati ambapo yeye na wafalme walikuwa wanakunywa katika mahema yao, na akawaamuru watu wake, “Jiandaeni kushambulia.” Kwa hiyo wakajiandaa kuushambulia mji.

Ahabu Amshinda Ben-Hadadi

13Wakati ule ule nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Je, unaona jeshi hili kubwa? Nitalitia mkononi mwako leo, nawe ndipo utajua kwamba mimi ndimi Bwana.’ ”

14 dAhabu akauliza, “Ni nani atakayefanya hili?”

Nabii akamjibu, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Maafisa vijana majemadari wa majimbo watafanya hili.’ ”

Akauliza, “Ni nani atakayeanzisha vita?”

Nabii akamjibu, “Ni wewe.”

15Kwa hiyo Ahabu akawaita maafisa vijana majemadari wa majimbo, wanaume 232. Kisha akawakusanya Waisraeli wote waliobaki, jumla yao 7,000. 16 eWakaondoka wakati wa adhuhuri, Ben-Hadadi na wale wafalme thelathini na wawili walioungana naye walipokuwa katika mahema yao wakilewa. 17Maafisa vijana majemadari wa majimbo waliondoka kwanza.

Wakati huu Ben-Hadadi alikuwa amewatuma wapelelezi, ambao walileta taarifa kusema kwamba, “Askari wanasonga mbele kutoka Samaria.”

18Akasema, “Ikiwa wamekuja kwa amani, wakamate wakiwa hai; ikiwa wamekuja kwa vita, wakamate wakiwa hai.”

19Wale maafisa vijana majemadari wa majimbo wakatoka nje ya mji jeshi likiwa nyuma yao, 20kila mmoja akamuua adui yake. Hii ilisababisha Waaramu kukimbia, huku Waisraeli wakiwafuatia. Lakini Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akatoroka akiwa amepanda farasi wake pamoja na baadhi ya wapanda farasi wake. 21Mfalme wa Israeli akasonga mbele na kushinda farasi na magari ya vita na kusababisha hasara kubwa kwa Waaramu.

22 fBaadaye nabii akaja kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Jiandae vizuri ufikirie la kufanya, kwa sababu mwakani mfalme wa Aramu atakuja kukushambulia tena.”

23Wakati ule ule, maafisa wa mfalme wa Aramu wakamshauri, wakamwambia, “Miungu yao ni miungu ya vilimani. Ndiyo sababu walikuwa na nguvu sana kutuzidi. Lakini kama tukipigana nao katika nchi tambarare, hakika tutawashinda. 24Fanya hivi: Waondoe hao wafalme wote thelathini na wawili kutoka nafasi zao na uweke maafisa wengine mahali pao. 25Ni lazima pia uandae jeshi jingine kama lile ulilopoteza, farasi kwa farasi, gari la vita kwa gari la vita, ili tuweze kupigana na Israeli katika nchi tambarare. Kisha kwa hakika tutakuwa na nguvu kuliko wao.” Akakubaliana nao naye akashughulika ipasavyo.

26 gMwaka uliofuata, majira kama hayo, Ben-Hadadi akawakusanya Waaramu mpaka Afeki kupigana dhidi ya Israeli. 27Baada ya Waisraeli kukusanywa na kupewa mahitaji, walikwenda kukabiliana nao. Waisraeli wakapiga kambi mkabala nao kama makundi mawili madogo ya mbuzi, wakati Waaramu walienea katika nchi yote.

28Mtu wa Mungu akaja na kumwambia mfalme wa Israeli, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Kwa sababu Waaramu wanafikiri Bwana ni Mungu wa vilimani na sio Mungu wa mabondeni, nitatia jeshi hili kubwa mkononi mwako, nawe utajua kuwa mimi ndimi Bwana.’ ”

29Kwa siku saba walipiga kambi wakitazamana na siku ya saba vita vikaanza. Waisraeli wakawajeruhi askari wa miguu wa Waaramu 100,000 kwa siku moja. 30 hWaliobaki wakatorokea katika mji wa Afeki, mahali ambapo watu 27,000 waliangukiwa na ukuta. Naye Ben-Hadadi akakimbilia mjini na kujificha kwenye chumba cha ndani.

31 iMaafisa wake wakamwambia, “Tazama, tumesikia kwamba wafalme wa nyumba ya Israeli wana huruma. Twendeni kwa mfalme wa Israeli tukiwa tumevaa nguo za gunia viunoni mwetu na kamba kuzunguka vichwa vyetu. Huenda akakuacha hai.”

32Wakiwa wamevaa nguo za gunia viunoni mwao na kamba kuzunguka vichwa vyao, walikwenda kwa mfalme wa Israeli na kusema, “Mtumishi wako Ben-Hadadi anasema: ‘Tafadhali, naomba uniache hai.’ ”

Mfalme akajibu, “Je, bado yuko hai? Yeye ni ndugu yangu.”

33Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!”

Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita.

Ben-Hadadi akajitolea, akisema,
34 j“Nitairudisha ile miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Unaweza kuweka maeneo yako ya soko katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya huko Samaria.”

Ahabu akasema, “Katika misingi ya mkataba, nitakuachilia huru.” Kwa hiyo akaweka mkataba naye, akamruhusu aende zake.

Nabii Amlaumu Ahabu

35 kKwa neno la Bwana, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.

36 lKwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Bwana, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.

37Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige tafadhali.” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi. 38Ndipo nabii akaenda na kusimama barabarani akimsubiri mfalme. Akajibadilisha kwa kushusha kitambaa cha kichwani mwake hadi kwenye macho. 39 mMfalme alipopita pale, yule nabii akamwita, “Mtumishi wako alikwenda vitani wakati vita vilipopamba moto, mtu mmoja akanijia na mateka akasema, ‘Mlinde mtu huyu. Kama akitoroka itakuwa uhai wako kwa uhai wake, ama vipande 3,000 vya fedha.’ 40 nWakati mtumishi wako alipokuwa na shughuli nyingi hapa na pale, yule mtu akatoweka.”

Mfalme wa Israeli akasema, “Hiyo ndiyo hukumu yako. Wewe umeitaja mwenyewe.”

41Kisha yule nabii akajifunua macho yake haraka, na mfalme wa Israeli akamtambua kama mmoja wa manabii. 42Akamwambia mfalme, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo: ‘Umemwacha huru mtu niliyekusudia afe. Kwa hiyo ni uhai wako kwa uhai wake, watu wako kwa watu wake.’ ” 43 oKwa uchungu na hasira, mfalme wa Israeli akaenda kwenye jumba lake la kifalme huko Samaria.
Copyright information for SwhKC